DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: JINSI GANI YA KUWA NA UJASIRI KATIKA KAZI

JINSI GANI YA KUWA NA UJASIRI KATIKA KAZI

Kukosa ujasiri limekuwa ni tatizo ambalo limewafanya wengi kujichukia, kutofikia malengo yao, kutokupata kazi nzuri, na kushindwa kila wakati. Kwa kutokana na kukosa ujasiri wengine tumekuwa na ufanisi mdogo na mambo kutuendele vibaya kila wakati. Kwanini mtu anajichukia au kujisikia vibaya anapokosa ujasiri? Ni kwa sababu hali hii inatokea ndani ya mtu na kwa jinsi yoyote ile kuwezi kumlaumu yeyote yule bali wewe mwenyewe.

Mambo ya Kufanya

1. Jitahidi kuwa hodari wa kile unachokifanya (Be a master of your situations)

Kati ya vitu vikubwa vinavyomnyima mtu ujasiri katika chochote anachokifanya ni kukosa uhakika na utaalamu wa kile anachokifanya. Mfano, fikiri kuhusu dereva mwanafunzi “learner” akiwa barabarani, fikiri kuhusu mwalimu mwanafunzi anayekaguliwa akiwa darasani. Hata kama mara nyingine ni kweli hujui na hauna ujuzi, lakini kule kujitia moyo kwamba unaweza huongeza ujasiri ndani ya mtu. Kibaya zaidi; ni kwamba wengi wetu huanza na sentensi ya “sijui” au “sintoweza” badala ya kuanza kwa kusema “hatakama sifahamu kwa sasa naweza kujifunza” au kusema nitaweza”.

Kuwa na lengo la kile unachotaka kukipata katika kazi fulani. Jiamini wewe mwenyewe na kiamini kile unachoweza kukifanya. Fanya kile ulicho kusudia kukifanya tena kifanye kwa akili zako zote. Kuwa mgunduzi, fanya kitu cha zaidi ya kile ulichokisomea shuleni au chuoni, matatizo ya dunia hii yote hayatatuliwi tu kwa ile elimu uliyoipata shuleni, tumia vipawa na karama alizokupa Mungu. Katika kulifanya lile unalolifanya chochote chaweza kutokea katikati ili tu kukukatiza au kuondoa malengo yako, jali zaidi kile unachokifanya, elekeza macho na akili zaidi katika kile ulichopanga  kukifanya na si vinginevyo.

Hata siku moja usifanye kazi kwa mtindo wa zimamoto, unasubiri muda karibu uishe, au muda wa kukabidhi kazi ufike “deadline” ndiyo unaanza kufanyakazi. Epukana na msongo wa mawazo, usisahau kuwa ubongo wa mwanadamu kufanya kazi vema na kwa ufanisi mkubwa pale ubongo huo unapokuwa umetulia na wakati huu ndiyo mzuri  wa kufanya yale yote yaliyo ya muhimu.

2. Kuwa mtu wa matendo (mtu wa kufanya) na sio mtu wa maneno matupu

Katika ulimwengu huu watu wanaweza kugawanywa katika makundi tofauti tofauti.

Kwanza: Kuna wale ambao hufanya vitu au mambo yatokee au yafanyike hawa ni wachache sana.

Pili: Wanafuatiwa na wale wanaoangalia tu mambo yakitokea.

Tatu: Wako wale ambao hungoja wenzao wafanye  halafu wao huanza kukosoa.

Mfanyakazi aliye jasiri, mwenye ujuzi na anayejiamini katika kila anachokifanya ni wa kundi la kwanza, wale wanaofanya mambo yafanyike. Wewe ndiyo wakufanya  kile unachokifanya kiwe kizuri na cha kuvutia, hakuna mambo ya kusema eti haya siyo mazingira mazuri kwa kazi hii au kazi fulani, jitihada zako zaweza kuyafanya mazingira hayo yawe ya kufaa.

3. Fanya kitu kimoja kwanza kabla ya kingine “Do one thing at a time”

Jifunze siri ya uwezo na kufikiria kwako, ubongo wako waweza kufanyakazi vema ikiwa utajua mfumo mzima wa kufikiri. Kamwe usiruhusu kuzama kwenye fikra tofauti na kile unachokifanya muda huo.  Weka mawazo na fikra zako katika kazi yako, usiruhusu mawazo yako kutoka nje ya kile unachokifanya. Hii ndiyo sababu tukiwa watoto tulifundishwa kufunga macho wakati wa sala, je unafikiri ni kwasababu maandiko matakatifu yametuagiza tufumbe macho? La hasha. Ni ili kutusaidia kuweka mawazo yetu yote, akili zetu pamoja na fikra zetu kwa yule tunayemuomba “Mungu”.

Najua wako wenye uwezo wa kufanya vitu viwili au vitatu kwa mara moja, wakati huohuo anapika, anaangalia luninga na anatumia simu ya mkononi, Hii inawezekana na ni sawa, lakini ufanisi katika haya yote waweza kuwa mdogo au kuhatarishwa. Haina haja na sio jambo la kiafya kuuchosha ubongo wako bila sababu za msingi. Katika hali hizi waweza kupoteza vyote na sio kimoja tu, jifunze kuangalia ubora wa kile unachokifanya na sio wingi wa kile unachofanya.

4. Kila siku jiweke wa kisasa zaidi, hasa katika ulimwengu huu wa teknolojia unaobadilika

Katika ulimwengu huu hakuna kitu kinachobaki vile vile kilivyo baada ya muda fulani. Kila kitu kinabadilika siku hizi kwasababu ya teknolojia, na kitu kimoja tu kisichokaa kibadilike kamwe ni ule ukweli kwamba “kila siku ni siku ya kujifunza”. Sababu ni kwamba kila mtu ambaye hakubali kuwa tayari kujifunza basi anabaki kuwa mzee kila siku hata kama ana miaka 20 au 30. Kila anayependa kujifunza, huyo huwa kijana kila siku (hazeeki).

Mtaalamu mmoja maarufu anaitwa Henry Ford alisema “The Greatest thing in life is to keep your mind young”. Kitu kikubwa na cha maana duniani ni mtu kiuruhusu akili yake kuwa ya ujana  kila siku. Hembu jisikie vizuri pale unapojifunza kitu kipya kila siku. Penda na jitahidi kujua mambo yanavyokwenda na yanavyobadilika kila siku. “Be current”. Jiulize ni nini usichokijua wakati wako wanaokijua zaidi yako.

5. Jifunze kuwasiliana vema na wenzako

Mawasiliano bora kati yako na wale unaofanyakazi nao yatakujengea ujasiri. Ili mawasiliano yawe bora ni lazima ujumbe tarajiwa ufike kwa mlengwa sahihi. Jumbe fupi na zisizokamilika hazijengi mawasiliano bali kupotosha maana na kutafsiriwa tofauti. Hii yaweza kuleta migongano, hakikisha umeeleweka kwa kile ulichotaka kukielezea. Ruhusu maelezo pale ambapo haujaeleweka na hujaelewa, usiwadharau waulizaji, maana sio wajinga bali hawajaelewa bado. Ruhusu misimamo yako ieleweke kwa wote mnaofanya kazi nao. Simamia kanuni zako na wala sio kuangalia sura ya mtu.

Na: Dr. Chris Mauki

Email: [email protected]

www.chrismauki.co.tzDr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *