DARASA LA ALHAMISI DR. CHRIS MAUKI: HATUA TANO ZA PENZI

HATUA TANO ZA PENZI

(Ingawa wengi huishia hatua ya tatu)

“Inawezekana hakuwa wakwangu”, “Yamkini Mungu hakupanga tuwe pamoja”, “Labda Mungu ameniepushia mengi”. Mara kwa mara wengi tumesikia sentensi zinazofanana na hizi hususani kwenye vinywa vya watu, marafiki au ndugu zetu ambao wamewahi kuachana, kutengana au kuvunja mahusiano. Au labda tumezisema sentensi hisi sisi wenyewe na wengine tunaendelea kuzisema hata sasa. Pamoja na kukiri maneno haya wapo watu ambao walikuwa wanawaangalia wewe na huyo aliyekuwa mpenzi wako na kuwaona mnaoendana sana “perfect couple”. Yamkini wewe mwenyewe umewahi kuona au kuhisi hivyo kwamba mimi na mpenzi wangu kwakweli tunaendana sana na labda tutaishi milele ingawa sivyo ilivyokuwa. Kila mmoja wetu hushangaa na kuchanganyikiwa akifikiria kwanini mapenzi ambayo yanaonekana kunoga kiasi hiki yanaishia kwenye machungu na majuto kiasi hiki. Kwanini muda mzuri tuliouwekeza kwenye mioyo ya wapenzi wetu unaishia kupotea kihasara namna hii? Jambo hili huwatatiza wengi sana na yamkini wewe ni mmoja wao. Tafiti za kisaikolojia kwenye eneo la mahusiano pamoja na yale mengi tunayokutana nayo kwenye kuwashauri wapenzi na wanandoa wengi yametufanya kufikia hitimisho kwamba mapenzi huwa yana hatua zake, na kwa bahati mbaya wapenzi wengi wanashindwa kuziendea hatua hizo moja baada ya nyingine badala yake wanaishia njiani, kama nilivyosema kwenye utangulizi kwamba wengi huishia hatua ya tatu. Fuatana nami katika makala hii uzielewe vizuri zaidi hatua hizi zitakazokusaidia sana.

 

Hatua ya kwanza: Kuingia katika penzi (Falling in love)

Hii ni hatua ya mwanzoni kabisa wakati umekutana na mtu ambaye unaona kama ni ndoto yako imekuwa dhahiri. Mtu uliyemtamani kwa muda mrefu sana. Hapa unajihisi mwenye furaha kuliko mtu yeyote yule. Hisia zako zote zinatawaliwa na mihemko ya kuwa na huyo unayemfia. Kila wakati na kila sehemu unatamani kuwa na huyo. Unamwona na kumuhisi yeye kuwa vyote katika vyote kwenye maisha yako. Hata afanye kosa la aina gani wewe unaliona ni jema tena lenye kuvutia. Hata kama ni mchafu na mwenye harufu mbaya wewe hautoona hilo kamwe. Hii ndio hatua ambayo binti huambiwa kwamba huyo kijana anayekuchumbia ni mwizi au ana wanawake wengi na akajibu “kwani hata mimi si mwanamke?” na wengine ukiwaambia mabaya ya kweli ya wapenzi wao wanakwambia Mungu atambadilisha. Hapa daima utamwamini huyo mpenzi wako katika kila asemalo hata kama unaambiwa uongo, na pia moyoni mwako unahisi kwamba huyo mtu anauwezo wa kuzitimiza ahadi zote alizokwambia na kila matamanio na ndoto zako anauwezo wakukuletea. Katika hatua hii hauko tayari kurudishwa nyuma na mtu yeyote, awe mzazi wako, ndugu yako wa damu, walimu wako, mchungaji au shehe wako au hata Mungu mwenyewe. Unachojua ni kimoja tu. Nampenda huyu, basi.

 

Hatua ya pili: Kuwa wawili (Becoming a couple)

Katika hatua hii mapenzi yamepevuka sana na ile mikutano ya hotelini, kwenye migahawa au kutembeleana mara kwa mara inabadilishwa kwa kuamua kuanza kuishi pamoja. Sasa hapa kama ni watu wa dini ndio watafunga ndoa za makanisani au misikitini, wengine bomani, wengine za mila n.k ili mradi waanze kuishi pamoja kama mke na mume. Kufahamiana kunazidi na unaanza kumjua mwenzako kwa kina zaidi hususani baadhi ya vitu ambavyo mwanzoni ulishindwa kuvijua kuhusu yeye. Uwepo wako unaanza kuwa na umuhumu mkubwa kwenye maisha ya mwenzako. Ndani yenu mnaanza kuhisi umoja na furaha ya kipekee. Kila kitu kikienda sawa, baada ya miezi au miaka michache kipindi hiki kinaweza kuwaleteeni mtoto ambaye anaweza kuiongeza furaha baina yenu. Hapa mwanamke anajihisi salama zaidi ya wakati akiwa hana mtoto na mwanaume anajiona anajukumu la kuwalinda mama na mtoto. Hisia za kuyapenda majukumu huanza na ulazima wakujibidisha huongezeka. Mara nyingi furaha na ule umoja inapoongezeka kila mmoja anahisi hakukosea kumpenda mwenzake na kwamba kila mmoja amekuja kwenye maisha ya mwenzake kwasababu sahihi.

 

Hatua ya tatu: Machungu ya kuhisi ulikosea (Disillusionment)

Katika hali ya kushangaza kabisa, katika kipindi hiki upepo unaanza kubadilika na kama ni safari ya baharini basi mnaanza kuona mawimbi yakivuma kwenye chombo chenu. Ndani yako unaanza kuona yale matumaini uliyokuwa nayo kwenye hatua ya kwanza nay a pili yanaanza kuzama. Kuna vitu zamani ulikuwa ukiviona vidogo tu kwenye tabia za mwenzako, ulikuwa ukiviona kama njiti, sikuhizi unaanza kuviona vikubwa kama misumari, na vinakuchoma kama moto. Vipindi vya hasira, kelele na kufokeana vinaanza kuingia kwenye mahusiano yenu. Ila kwa mbali moyoni mwako au akilini mwako unaweza kuwaza labda iko siku hisi hisia zitaniisha ili nirudi kumpenda tena huyu mume au mke wangu. Katika kipindi hiki wengi wanatoa sentensi za “tuachane kama tumeshindwana”, “kama umenishindwa nirudishe kwetu”, “nikirudi nisikukute” n.k. Kiukweli katika hali na upepo huu ndani yako unahisi kabisa kwamba ulikosea kumchagua yeye, na wengine wanajutia kabisa uamuzi wao wa kuamua kuoana na yeye. Zile hisia za kumpenda, kumlinda, kumfurahisha na kumtetea mpenzi wako zinaenda na maji mbali kabisa, tena hutaki kabisa kumsikia, unatamani hata asirudi nyumbani kwa jinsi anavyokuudhi. Kama mwanzoni mlikuwa mnafurahia tendo la ndoa basi sasa ndio tendo hilo linaingia shubiri. Hutaki akuguse wala akusogelee. Kwa bahati mbaya vita hii na kutofautiana huku kunapozidi uwezekano wa michepuko huongezeka ambayo na hiyo huongeza vita na mchimbiko pale ambapo kunakugundulika. Katika kipindi hiki kiu ya kuwa pamoja imekufa na kuzikwa kabisa, wengine wanatafuta maeneo ya kupumulia ilimradi asiwe nyumbani, wakushinda baa ndio anapotelea huko kabisa, wakushinda kazini ndio atakaa huko hadi usiku wa manane kama vile mfanyakazi bora kumbe ana maumivu, wakushinda makanisani basi ndiyo utadhani kaambiwa Yesu anarudi kesho kumbe anamkimbia mwenza wake. Yani kushoto na kulia kote kunakuwa shubiri.

 

Hatua ya nne: Kutengeneza penzi la kweli linalodumu

Kwa bahati mbaya ndoa za wengi zimeishia hatua ya tatu, na yamkini wakati unasoma makala hii unajijua fika kwamba yakwako iliishia hatua ya tatu wewe ukidhania kwamba ulivumilia sana na ulijitahidi sana lakini ukashindwa kumbe ukweli nikwamba bado safari ilikuwa bado inaendelea. Kama kweli uliweza kuvumilia na kufumba macho ukikabiliana na kila upepo kwenye hatua ya tatu. Ukavumilia matusi, kupigwa na kudharauliwa. Ukastahimili aibu ya kukalishwa vikao mbele ya ndugu, wasimamizi wa ndoa, marafiki na hata viongozi wa dini. Yamkini ziko nyakati ulirudishwa kwa wazazi wako lakini mkayaongea ukarudi kwako, zipo nyakati alikwambia haufai uondoke hakutaki lakini aliporudi alikukuta umemwandalia chakula na maji ya kuoga umemwekea. Yamkini ulidharauliwa na kudhihakiwa na wengi wakisema utapigwa hadi ufe, wewe ukabaki kutokusikiliza vinywa vya watu ukamwangalia Mungu tu. Inawezekana ulikubali kutokuheshimiwa kama baba na mume na ukarushiwa maneno ya nguoni na kudhalilishwa mbele ya watoto lakini ukajipa moyo ukisema huyu ni mama wa watoto wangu nitamlinda. Kama ulipenya kote huko basi unaingia kwenye hatua ya nne. Hatua ya kulitengeneza penzi la kweli na linalodumu. Katika hatua hii moyo wako unaondokana na zile hisia hasi za kujiona uliye kosea kuwa na huyo mwenza wako. Huyo mpenzi unayemwona mbele yako unajutia kumtendea kila hiana miezi au miaka michache iliyopita maana sasa ukimtazama unamwona kama malaika kwako. Sasa unaanza kumwelewa sana na kuyakubali mapungufu yake. Huu unakuwa wakati wa kuponya majeraha na kuingia kwenye hatua ya mwisho.

 

Hatua ya tano: Nguvu ya wawili inatumika kubadili ulimwengu

Sasa umeshaweza kumfahamu vema mwenzako na hakuna kinachokuyumbisha kwa urahisi  maana tayari misuli yako ya uvumilivu, ustahimilivu umetanuka. Sasa unaweza kabisa kustahimili kutofautiana, na hata kuwepo na hisia hasi bado unaweza kupenyeza upendo kwa mwenzako na akauona dhahiri upendo huo. Hapa mnajisikia huru zaidi, kuhitajiana zaidinakuhusiana zaidi. Mnaihisi nguvu ya kuleta mabadiliko makubwa sio tu baina yenu bali na kwa wengine wengi wanaowazunguka. Kuhusiana kwenu sasa hakuwi tu kwasababu ya kuzifurahisha hisia zenu bali kwasababu ya kusudi kubwa ambalo mnahisi Mungu ameliweka ndani yenu. Maranyingi wengi kwenye muda huu wanafanya kazi nyingi pamoja, wanalima pamoja, wanaandika pamoja, wanafundisha pamoja, wanahubiri pamoja au kufanya mengi mengine kwa pamoja. Ile nadharia ya mwili mmoja ndio inakuja kuwa dhahiri wakati huu na baada ya kupita kwenye hatua zote nne za nyuma sasa unaujasiri usiofichika ndani ya moyo na kinywa kutamka kwamba “Huyu ndiye Mungu aliyenipa”. Ni maombi yangu na dua yakwamba kila mtu, hususani wewe unayesoma makala hii uifikie hatua hii. Nakutakia kila laheri.

 

Imeandaliwa na;

Dr. Chris Mauki

Mhadhiri na mtaalamu mshauri wa saikolojia

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

[email protected]

www.chrismauki.co.tz

 

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *