DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: MBINU ZA KUKUSAIDIA KUSHUHULIKIA MOYO ULIOUMIA “DEALING WITH A BROKEN HEART”

MBINU ZA KUKUSAIDIA KUSHUHULIKIA MOYO ULIOUMIA

“DEALING WITH A BROKEN HEART”

Mwandishi wa masuala ya mahusiano Bess Myerson amewahi kusema kwamba kutumbukia kwenye penzi ni kitu rahisi sana lakini kuchomoka kwenye penzi ni mtihani mgumu sana kwa wengi, tena sio mgumu tu bali wenye maumivu na majeraha mengi. Ni kweli kwamba maumivu na changamoto zinakuwa ngumu zaidi pale ambapo wewe ndiye uliyekuwa unatamani sana penzi lenu lidumu. Pamoja na maumivu na ugumu ulioko katika kulazimika kuvunja penzi lililokuwepo bado hauwezi kusema sinto penda tena au sinto pendwa tena au sitaki mapenzi tena, huko kutakuwa ni kutokujitendea haki. Mwandishi Henri Nouwen amewahi kusema maneno ambayo kila siku ninakubaliana nayo, kwamba “pale ambapo waliowahi kukupenda sana watakapokukataa, watakapo sitisha kukupenda au watakapo ondoka duniani moyo wako utaumia na kupondeka sana. Lakini hiyo haikuzuii usijekupenda sana. Maumivu yaliyotokana na kuumizwa baada ya kupenda kwa kina yanaweza kukufanya ujekuzama kwenye penzi”. Swali ni kwamba, tunatokaje kwenye maumivu haya makali? Hapa nakuletea mbinu kadhaa nilizozipata kwenye wataalamu mbali mbali wa mahusiano na pia katika kuzungumza na watu mbali mbali waliopitia changamoto hizi na wakajikusanya na kuendeleza maisha tena katika mapenzi makubwa zaidi.

 

1. Hakikisha unakubali kukatiza katikati ya hilo tatizo na sio kulizunguka

Nimegundua kwamba mtihani mgumu kwa mtu aliyeumizwa moyo ni kusimama imara na kuyasikilizia maumivu au kule kuumizwa pasipo kujifanya kama vile hakuna kinachotokea. Ukweli ni kwamba hivyo ndivyo mtu anayotakiwa afanye, kwasababu hakuna njia ya mkato pasipo kuyahisi, kuyapitia na kuyamaliza maumivu ili upone. Ni lazima upitie maombolezo na kuyamaliza ili uweze kuendelea na maisha yako. Kwanini ninakushauri uyapitie maumivu yako na kuyamaliza na sio kuyazunguka tu, hii ni kwasababu kama ukiyaogopa na ukayazunguka mduara au ukiyakwepa, utadumu hapo kwa muda mrefu sana ukizania umepona kumbe bado, na kuna uwezekano mkubwa huko mbele ya safari utakutana na yale yale uliyokuwa unayakwepa. Katika hali hii usidhani kwamba umemaliza maumivu, la hasha. Kwa kuyakubali maumivu na kule kuvunjika moyo na kuamua kupitia halihiyo kiuhalisia kunakuimarisha ndani yako na kukufanya thabiti katika kumalizana na ungwe hiyo ya maumivu na majeraha ya ndani. Mara unapomaliza kipindi hicho unakuwa huru, tena huru kabisa na unakuwa umeiangusha ile ngome ya maumivu kukutesa.

 

2. Simama imara na simama pekeyako

Kati ya vitu unavyotakiwa kuvifahamu unapopitia kwenye machungu moyoni ni kwamba hauhitaji mtu yeyote au kitu chochote kukupa furaha, kazi hiyo ni yako wewe pekeyako pamoja na msaada kutoka kwa Mungu. Maranyingine inakuwa ngumu sana unapopitia maumivu makali kwenye mapenzi kuamini kwamba unaweza kuvuka pasipo msaada au pasipo uwepo wa yule unayeamini unamhitaji katika maumivu hayo, lakini ukweli ni kwamba unaweza kusimama peke yako, tena unaweza sana tu. Ni kazi yako kuujaza ule uwazi au utupu ndani yako, ni kazi yako kuitia miguu yako nguvu ili usimame mwenyewe. Ukisimama mwenyewe na ukitegemea nguvu za aliyejuu utashangaa kuwa unaweza.

 

3 Jinasue

Jitihada za wewe peke yako kuujaza uwazi ulionao moyoni mwako uliosababishwa na maumivu, pasipo kukimbilia kujiingiza kwenye mahusiano mapya kwa haraka au kujaribu kushindana ili umrudishe huyo mpenzi wako aliyekwishaondoka, huko ndiko tunakokuita kujinasua. Utakubaliana na mimi kwamba wako wengi ambao kwa kukwepa kustahimili maumivu ya hisia na kwa kushindwa kujinasua huamua kujiingiza kwenye mahusiano na mpenzi mwingine haraka hata kabla mtu hajapona, wengine hufanya hivi ili tu ajiliwaze, au akidhani penzi jipya la ghafla litamsaidia kupooza machungu ya penzi lililokufa, wengine hutaka kufanya kwa kulipiza kisasi, lakini wengi wa mazingira ya namna hii wamejuta baada ya muda mfupi sana. Maranyingine unaona kabisa kwamba mwenzako amekuacha, na hakuna dalili za yeye kuwa na wewe tena, labda amekwishaoa, au anampenzi mwingine, au amekuhakikishia kwamba anataka kuwa na maisha mapya bila wewe, lakini kwasababu wewe unaona hauweze kamwe kuishi bila yeye, basi hukubaliani na hilo, kila siku unamtafuta kwenye simu, kila wakati unamwandikia barua pepe, kila wakati unachimbua maisha yake ujue leo yuko wapi na anafanya nini na nani, kwa kufanya hivyo haujui ya kwamba unachelewesha mchakato wa kupona kwako na kujinasua kutoka maisha ya aliyekuacha. Kamwe hautoweza kuwa na uhuru binafsi mbali na maumivu ya moyo na hisia kama hautoweza kujinasua.

 

4. Andika yale mambo unayoyaweza “list your strengths”

Pamoja na kwamba umetumbukia kwenye maumivu makali ya moyo na hisia. Pamoja na kwamba ndani yako unahisi hakuna anayeumia kama wewe kwa sasa. Pamoja na kwamba unajiona usiyefaa na usiyeweza chochote, bado yako mambo mengi unayaweza na waweza kujitahidi kuyafanya kwa kiwango kizuri sana. Hembu kaa chini uyaandike mambo hayo, hembu kaa ujikumbushe kwamba kule kushindwa jambo moja sio kwamba kunamaanisha wewe huwezi kabisa. Jiulize ulisha wahi kuvumilia mamngapi, tena labda makubwa kuliko hilo unalopitia, jiulize umeshawahi kupata hasara ngapi? Umesha wahi kupoteza marafiki wangapi na ukasimama thabiti na maisha yakasonga? Jiulize umesha wahi kusifiwa kwa kufanya vizuri mara ngapi? Umeshawahi kuwashauri walioumia moyo marangapi na mambo yao yakakaa sawa? Kumbe hili unalopitia sasa bado unanguvu ndani yako ya kulisukuma lipite ili maisha yako yaendelee. Kama unaamini kabisa kwamba hakuna jema na zuri unaloliweza au ulilowahi kulifanya basi tatizo ni kubwa kwako zaidi ya unavyodhani. Na Yamkini tatizo sio tu hayo maumivu unayoyapitia sasa.

 

5. Maranyingine ruhuru fikra kuhusu yule aliyekuumiza

Usidhani kwamba kwa kuzuia mawazo yako yasimfikirie au huyo mtu asikujie akilini au moyoni ndio kulitatua tatizo, unaweza kukuta kwa kufanya hivyo ndio unaongeza machungu kwasababu utaumia zaidi pale utakapoona mtu huyo anakuja kwa kasi au kwa lazima akilini mwako bila ruhusa yako. Kwa kulifahamu hili na kwa kujua kwamba hii ni hali ya kawaida katika saikolojia ya nafsi ya mwanadamu basi tunakushauri uruhusu fikra hizi kukujia, usilazimishe kujenga ukuta nafsini mwako ili zisikujie. Yamkini ziko nyakati utamkumbuka mlivyokuwa mnafurahia nyakati za pamoja, yamkini utakumbuka vitu alivyokupa au ulivyompa, au utawaza hivi kama akirudi tena nitafurahia naye kiasi gani? na yamkini utakumbuka nyakati chungu pia. Hii yote ni sawa na sio dhambi. Ikumbukwe kwamba hapa sisemi ukeshe ukimvuta huyo mtu akilini mwako ila namaanisha pale fikra zake zinapokujia kwa lazima usipingane nazo.

 

6. Jitahidi kumsaidia mwingine

Mara nyingine njia ya kutoka kwenye maumivu makali ya moyo au nafsi ni kuzipeleka nishati zako katika kumsaidia mtu mwingine katika mazingira mengine. Pale unapojeuza hisia zako na mtazamo wako kuelekea kumsaidia mtu mwingine ambaye anapitia pagumu kama wewe, kunakufanya usahau kuhusu shida zako japo kwa kitambo kidogo. Mara nyingine kule kuondokana na kukesha kuwaza na kulifikiria lile linalokuumiza hata kama ni kwa dakika chache sana bado inakuwa ni muujiza kwako, kwahiyo jaribu kuzipeleka hisia zako kwenye kutoa msaada kwa mwingine na kuifikiria shida yake ili uupumzishe moyo na nafsi yako kwenye kuliwaza tatizo lako.

 

7. Pata nyakati za kucheka na kulia

Kucheka ni dawa katika maeneo mengi sana, na kulia pia ni dawa katika maeneo mengi. Labda umewahi kushangaa kwanini kuna nyakati unaumia moyo sana na ukishalia kwa uchungu unajisikia nafuu kubwa sana kihisia. Hii inakuonyesha wazi ni kwa jinsi gani ipo nguvu ya uponyaji kwenye machozi. Mtaalamu na mtafiti wa baiolojia na kemia bwana William Frey aliyetumia miaka 15 katika utafiti kuhusu machozi anasema machozi yanayomtoka mtu kwa kusababishwa na maumivu ya hisia huambatana na kemikali zenye sumu “toxic biochemical byproducts”na jambo hili lina maanisha kwamba kwa kulia pale unapoumia moyo au hisia unaachilia kekikali zisizohitajika au ambazo zingeleta madhara mwilini na pia kukusaidia kuondokana na hali ya juu ya msongo wa mawazo. Kwahiyo ushauri wangu kwako ni kwamba, unapohisi kutaka kulia kwasababu ya maumivu ya hisia wala usijizuie. Lia, tena lia hadi utakapoona unautua mzigo.

 

Dr. Chris Mauki

University of  Dar es Salaam

chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.co.tz

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *